TABASAMU TAANUSI KWA WAPWANI!

                Wasemavyo walumbi nyumbani ni nyumbani tu hata kama ni pangoni na kitanda usichokilalia hujui kunguni wake.Imesadifika tu kama hekaya za Abunwasi kwetu sie wapwani huku tukisalia tumeduwaa na kubung'aa falauka mzungu wa reli tusiamini kutokana na furaha chekwachekwa iliojaa moyoni.Walilonga waswahili kuwa,lisemwalo lipo na kama halipo laja.Nakusihi uketi kitako ewe msomaji wangu nikudadavulie yaliyomo!
                     Ni miezi miwili tu tangie sie wapwani na wakenya kwa ujumla kushiriki kwenye uchaguzi mkuu wa agosti tisa huku kilio chetu wapwani kikiwa ni halwa tamu tulionyang'anywa kinywani na kupelekewa wakazi wa Naivasha kwenye nia ya huduma za halmashauri ya bandari nchini (KPA).Ama kweli chozi la samaki haliendi bure majini.
                 Nakumbuka tu kama jana jinamizi  lililotufyonza sie wapwani pindi tu  baada ya huduma za halmashauri ya bandari jijini Mombasa kupigwa teke na rais mstaafu Uhuru Kenyatta tukalazimisha  kusalia wapweke tusiwe na 'a' wala 'b'.Uchochole ukakita mizizi na kutufanya tukose hata tonge la kutia domoni kutokana na gharamu za maisha zilichangiwa na ukosefu wa ajira.Vijana tulilazimika kujiingiza kwenye gege la ugaidi ikiwemo uporaji na wizi wa kimabavu uliosababisha visa vingi  vya utovu wa usalama na uzorotaji wa kiuchumi, nikitaja tu baadhi.
                     Pongezi ewe amiri mkuu wa jeshi la kitaifa rais William Ruto kwa kutoa amri ya kurejeshwa kwa huduma za halmashauri ya bandari nchini kwa wakazi wa pwani.Heko kwako rais.Ni raha ilioje kwetu sie wapwani? Natumai shughuli za kawaida zitarejelewa huku wapwani tukinufaika kwenye halmashauri hiyo na kuimarisha maisha na uchumi wa ukanda huo huku nafasi za ajira zilizosambaratishwa zikitengwa upya.
                     Sie wapwani twawaomba washikadau wamfikishie shukrani rais William Ruto tukimsihi azidi kutekeleza ajenda alizoahidi wakenya bali si kwetu wapwani tu ili kufanikisha ustawishaji na uboreshaji wa uchumi wa taifa.Kila la kheri rais.
Ni mie Shem Felix Ashikumba, mwanafunzi kutoka kitengo Cha habari na mawasiliano, kwenye chuo kikuu Cha ufundi Mombasa (Technical University of Mombasa) TUM.
                     

Comments

  1. hongera kwa kazi nzuri

    ReplyDelete
  2. Tafsiri nzuri na yenye ufasaha. Hongera.

    ReplyDelete
  3. Thanks all for the support 🙏🙏

    ReplyDelete

Post a Comment

Popular posts from this blog

CHOZI LA DAMU!

VIJANA TAMBARANI!